
Zanzibar, 3 Juni 2025 – Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mheshimiwa Lela Muhammad Mussa, leo ameongoza hafla ya kuwaaga wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya awamu ya tano ya Maamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar, na kuzindua rasmi bodi mpya itakayosimamia shughuli za taasisi hiyo.
Hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa ofisi kuu ya Maamlaka hiyo huko Unguja, na kuhudhuriwa na viongozi wa serikali, watendaji wa Mamlaka, wajumbe wa bodi wapya na wastaafu na wadau wa elimu ya amali.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mheshimiwa Lela aliipongeza bodi iliyomaliza muda wake kwa kazi kubwa waliyofanya katika kipindi cha miaka mitatu (Februari 2022 – Februari 2025) katika kuimarisha maendeleo ya Maamlaka hiyo. Amesema mafanikio hayo yamekuwa chachu ya utekelezaji wa sera ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuwawezesha vijana kupitia elimu ya amali.
Aidha, Mhe. Lela aliwataka wajumbe wa bodi mpya kufanya kazi kwa mshikamano, weledi na ubunifu katika kusimamia utekelezaji wa mipango ya taasisi hiyo. Alisisitiza umuhimu wa kutumia vyombo vya habari katika kutoa elimu kwa jamii juu ya nafasi ya vyuo vya amali katika kuchochea maendeleo na kupunguza tatizo la ajira.
“Mitaala ya elimu inaendelea kufanyiwa mapitio ili kuongeza fani mpya za elimu ya ufundi zitakazowawezesha vijana kupata ujuzi wa vitendo unaohitajika katika soko la ajira na katika kujiajiri,” aliongeza Mheshimiwa Lela.
Mapema, Mkurugenzi Mtendaji wa Maamlaka hiyo, Dkt. Bakari Ali Silima, alimkaribisha rasmi Waziri Lela na kuipongeza bodi iliyomaliza muda wake kwa mafanikio makubwa, ikiwa ni pamoja na kusajili vituo vipya 64 vya mafunzo, kuanzisha fani mpya kama vile uvuvi, ufugaji na utalii, pamoja na ongezeko la vijana wanaojiunga na vyuo vya amali visiwani Zanzibar.
Kwa upande wake, Mwenyekiti Mstaafu wa Bodi ya Wakurugenzi, Mhandisi Khamis Adam Khamis, alieleza kuwa bodi hiyo imefanikiwa kutekeleza majukumu yake kwa kiwango kikubwa na kwa kuzingatia sera na vipaumbele vya Serikali. Aliongeza kuwa taasisi hiyo imekuwa nyenzo muhimu katika kuwajengea vijana uwezo wa kujitegemea kiuchumi kupitia mafunzo ya vitendo.
Bada ya hotuba hizo, Mwenyekiti mpya wa Bodi, Ndg. Madina Mjaka Mwinyi, ambaye ni Naibu Katibu Taaluma mstaafu katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali aliahidi kuendeleza juhudi za maendeleo ya Mamlaka hiyo huku akieleza kuwa changamoto ya rasilimali fedha bado ni kikwazo kwa baadhi ya miradi kufikiwa kwa wakati na katika kipindi chake atajitahidi kuitatua changamoto hiyo.
Waziri Lela aliizindua rasmi Bodi mpya ya Wakurugenzi na aliitakia mafanikio katika utekelezaji wa majukumu yake.
Hafla ilihitimishwa kwa zoezi la ugawaji wa vyeti na zawadi kwa wajumbe waliomaliza muda wao, ikiwa ni ishara ya kutambua na kuthamini mchango wao mkubwa katika kuiendeleza Mamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar.
Imetolewa na:
Kitengo cha Uhusiano – Maamlaka ya Mafunzo ya Amali Zanzibar.