Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imesema, inaunga mkono mpango ulioandaliwa na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume (KIST), katika utowaji wa mafunzo ya huduma za ndege katika Viwanja vya Ndege.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Bw.Khamis Abdalla Said, amesema hayo alipokuwa katika hafla ya utiaji saini makubaliano ya utowaji wa mafunzo hayo kwa Taasisi ya Karume na Wataalamu wa huduma za ndege katika viwanja vya ndege, hafla ilifanyika katika Ukumbi wa Mkutano wa Dkt. Idrissa Muslim Hijja Bweni Zanzibar.
Amesema, hatua hiyo inakwenda sambamba na dhamira ya Serikali juu ya kuimarisha usafiri wa anga hapa nchini.
Amesema, kuwepo kwa mafunzo hayo itachochea kupatikana Wafanyakazi wa kutosha wenye utaalamu wa kutoa huduma kwa kiwango kinachohitajika.
Aidha, Bw.Said amefahamisha kuwa, Vijana wengi wanamaliza elimu zao na kubakia mitaani kufanya mambo yasiostahiki hivyo, kuwepo kwa mafunzo hayo itakuwa chachu ya kutimiza ndoto zao na kuipunguzia mzigo Serikali.
“Hakuna sababu kwa huduma hizo kufanywa na wageni ukizingatia hapa nchini kuna vijana wengi hawana ajira hivyo kupitia fursa hiyo itakuwa chachu ya kuwasaidia vijana kupata nafasi hizo na kujikwamua kiuchumi,”alisema.
Hata hivyo amesema, Zanzibar inaendelea kujenga miundombinu na kujenga Viwanja vya Ndege Unguja na Pemba hatua ambayo itasaidia kuongeza idadi kubwa ya ndege kutoka nchi mbalimbali kufanya safari zake hapa nchini, hatua ambayo itatanua wigo na kuongeza fursa za ajira katika eneo hilo.
Amesema, kutokana na hali hiyo KIST inajukumu la kuhakikisha wanaandaa wataalamu watakaokuwa na uweledi ambao wataweza kufanya kazi hizo ndani na nje ya nchi.
Hivyo kawataka vijana kutumia fursa ya mafunzo inayotolewa na taasisi hiyo ili kupata taaluma na ujuzi katika soko la ajira katika sekta hiyo.
Hivyo ametumia fursa hiyo kuzitaka kampuni za ndege ziliyopo ndani na nje ya nchi, kuunga mkono jitihada za Serikali ya Zanzibar kwa kuwapa fursa za ajira vijana watakaosoma katika kozi hizo ili kwenda kufanya kazi katika sekta hizo.
Mapema Mkuu wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume (KIST), Dk.Mahmoud Abdulwahab Alawi, amesema, wamesaini makubaliano hayo kwaajili ya kuendesha kozi tofauti za utowaji wa huduma kwa kazi mbalimbali zinazofanyika katika viwanja vya ndege.
Amesema, hatua hiyo itasaidia kuwajengea uwezo wazawa kufanya kazi hizo kutokana na kuwepo idadi kubwa ya viwanja vya ndege na Makampuni mbalimbali kufanya safari zake hapa nchini.
Nae Mkuu wa Idara ya Uhandisi wa Mitambo na Usafiri wa Anga kutoka KIST Bw. Ali Hamad Mkali amesema, lengo la makubaliano hayo ni kuanzisha mafunzo ya muda mfupi ndani ya Taasisi hiyo kwa lengo la kuwaandaa vijana ili kuingia katika soko la ajira kupitia eneo hilo la utowaji wa huduma katika viwanja vya ndege.
Nae Mtaalamu wa Mafunzo hayo Ndugu. Hassan S. Ngozi amesema, watowa huduma za ndege wanahitajika kuwa na taaluma na uelewa ili kuepusha athari mbalimbali zinazoweza kujitokeza.
Mafunzo hayo ya muda mfupi yatashirikisha kozi mbalimbali ikiwemo usafirishaji wa mizigo, abiria, uangalizi wa mashine za kusafirishia mizigo na mengineyo.
Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano (WEMA).
Tarehe : 6/09/2023