WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar amewashauri, wazazi na  walezi wa skuli ya sekondari Wanawake ya Luther ya Bagamoyo, kuwa makini na malezi ya wao.


Akitoa kauli katika hutuba iliyosomwa kwa niaba yake na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Ali Abdugulam Hussein, wakati akizungumza katika mahafali ya 11 ya kidato cha nne yaliofanyika Bagamoyo.


Amesema mambo ya utandawazi na mmong’onyoko wa maadili, umesababisha vijana wengi kupata  matatizo ya afya akili na ukosefu wa nidhamu.


Amesema hali hiyo huchangia kwa kiasi kikubwa kujiingiza kwenye makundi ya matumizi ya dawa za kulevya, kutojitambua kwa baadhi yao, hivyo kuharibu nguvu kazi ya taifa kwa miaka ya mbele.

Ameongeza kuwa ni vyema kwa wazazi kuwashika mkono uongozi kwa kuwaleta watoto kwenye skuli hiyo ili waweze kutimiza malengo yao  ya kitaaluma.


Amewapongeza walimu na uongozi wa skuli hiyo kwa juhudi kubwa wanayofanya katika kufundisha na kufaulisha wanafunzi, hivyo amewashauri kuendelea kujituma katika kufanya kazi zao.


Mapema mwalimu mkuu wa skuli hiyo Beatrice Kiwelu amesema skuli hiyo imeanzishwa mwaka 2010 na hadi sasa ina wanafunzi 130.


Amesema skuli hiyo imekuwa ikifanya vyema katika mitihani yake ya taifa na ngazi nyingine, jambo ambalo linawafanya wazee kuvutiwa na skuli yao.


Naye mwakilishi wa wazazi Jennifer Mgendi amewapongeza wanafunzi kwa kukubali kusoma, kwani hivi sasa kumekuwa na kundi kubwa la wanafunzi ambao hupenda kujiingiza katika makundi maovu.


Amewataka wanafunzi kutoridhika na elimu walioipata badala yake waendelee kutafuta elimu zaidi ili iwasaidie katika maisha yao.