Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imewataka Wadau wa elimu kuwa makini katika kupanga mipango mizuri itakayowasaidia vijana waliokuwa hawamo kwenye mfumo wa elimu kuweza kujitegemea.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Dkt. Mwanakhamis Adam Ameir, ameeleza hayo alipokuwa akifungua mkutano wa siku moja wa kuandaa mpango kwa Zanzibar uliofanyika huko Madina Elbahar Mbweni Wilaya ya Magharib B Unguja.

Amesema, katika kupanga mipango hiyo ni vyema kwa wadau hao kuangalia ujuzi ambao vijana wa Zanzibar wanaoupenda na wenye kuleta tija kwa taifa na hatimae kuweza kujikwamua na tatizo la ajira.

Naibu katibu mkuu huyo amefahamisha kuwa,Serikali ya Awamu ya Nane kipaumbele chake ni dhana ya uchumi wa buluu hivyo ni vyema mipango na mikakati ambayo itapangwa iendane na dhana hiyo Zaidi.

Akizungumza katika mkutano huo Mratibu wa Mpango wa Elimu kwa ajili ya vijana waliokosa fursa ya kuendelea na masomo Tanzania (EPOSA)nd SIAFU SEMPERO amesema,katika kuhakikisha Zanzibar inaenda kufanikiwa katika mikakati yake ya kutekeleza mipango yao kwa vijana, ameshauri kuwaweka vijana hao kwa vikundi.

Nae Mwakilishi wa Shirika la Kimataifa la kusaidia Watoto Duniani (UNICEF) OUSMEN NIANG amesema, vijana ni kundi muhimu kwa maendeleo ya taifa hivyo ni vyema kupangiwa mikakati ambayo itawawezesha kulisaidia taifa lao.

Mkutano huo umewashirikisha watendaji kutoka wizara ya elimu na mafunzo ya amali Zanzibar,Taasisi ya Elimu ya watu wazimaTanzani na kufadhiliwa na UNICEF.

Imetolewa na kitengo cha Habari na Mawasiliano (WEMA).
Tarehe:26/09/2023