Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mhe. Zubeir Ali Maulid amesema, jitihada zinazochukuliwa na Serikali katika kujenga hamasa kwa Wanafunzi kusoma na kupata matokeo yaliyokuwa bora.
Ameyasema hayo alipokuwa akifungua Maonesho ya Juma la Elimu ya Juu kwa niaba ya Makamo wa Pili wa Rais huko Maisara, amesema, Maonesho hayo ni sehemu ya ubunifu wa Wizara ya Elimu katika kukuza huduma za kielimu.
Amesema, Serikali imekuwa inahitaji Wataalamu wa sekta mbali mbali ili kuendelea kufanya kazi nchini.
Amesema, hatua ya Wizara ya Elimu kuweka Maonesho hayo itafikiwa lengo ikiwemo Wanafunzi kujifunza kupitia Maonesho hayo ikiwemo kujua namna bora ya kujiunga na Vyuo mbalimbali vilivyopo nchini.
Hivyo, amewaomba Wanafunzi hao kuwa na mwamko mzuri wa kusoma ili kuona Taifa linaendelea kuwa na Wasomi waliokuwa na viwango vizuri kielimu na taifa liweze kupiga hatua zaidi kitaaluma.
Sambamba na hayo, amewaomba Wazazi na Wanafunzi kutembelea Maonesho hayo ambayo yatawapa kufanya maamuzi juu ya chuo sahihi kulingana na matokeo waliyoyapata ili kuendelea na masomo yao.
Mapema, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe. Ali Abdulgulam Hussein, amepongeza juhudi za Serikali katika kulipa umuhimu suala la Elimu na kupelekea kuwa na matokeo mazuri.
Aidha, amewapongeza Viongozi Wakuu kwa jitihada zao wanazozifanya katika kuona Elimu inaendelea kuimarika ambapo kwa sasa wameengeza bajeti ya fedha katiba Bodi za Mikopo kwa Wanafunzi wakiwa na lengo la kuona Wanafunzi wanasoma wakiwa katika mazingira mazuri.
“Viongozi hawa wamehakikisha Elimu wanaipa kipaombele, kwani wameweza kutoa Skolaship ambazo nafasi hizo wanakwenda kupatiwa vijana wa Tanzania ambao waliofanya vizuri katika mitihani yao” amesema.
Nae, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Bw. Khamis Abdalla Said, amesema, Wizara yao imepata bajeti kubwa jambo ambalo limeonesha wazi kuwa Rais Dk. Mwinyi amekuwa akichukua jitihada mbalimbali kuona viwango vya Elimu vinaendelea kukua nchini.
Amesema, Wataendelea kusimamia Walimu ili kuona ufaulu unaendelea kuengezeka sambamba na kuwasisitiza Wanafunzi kuendelea kusoma kwa bidii.
Maonesho hayo ya Nne yameshirikisha Taasisi za kielimu zipatazo 57 kutoka Taasisi 32 za mwaka uliopita
Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano (WEMA).