Naibu Katibu Mkuu Utawala Wa Wizara Ya Elimu Na Mafunzo Ya Amali (Wema) Ndg Khalid Masoud Wazir amesema wasimamizi wa miradi ya maendeleo ni vyema kujiandaa mapema ili kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza.
Ameeleza hayo katika mkutano wa kamati za kupokea malalamiko katika maeneo yatakayojengwa miradi ya maendeleo kupitia mradi wa kuwajengea uwezo vijana kujiajiri na kuajirika kupitia uchumi wa buluu (SEBEP) huko mpirani Mkoa wa Mjini Magaribi Unguja.
Naibu Khalid amefahamisha kuwa hatua hiyo pia itarahisisha ufanisi wa miradi hiyo na kumaliza kwa wakati.
Aidha amezitaka kamati hizo kuhakikisha zinasikiliza malalamiko ya wananchi ili kupatiwa ufumbuzi, na kuisisitiza jamii kuitunza miradi wanayojengewa kwa maendeleo yao na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake meneja wa mradi wa SEBEP ndg Salum Mkubwa amewataka wazazi na viongozi kuendelea kuwahamasisha vijana kujiunga na kozi mbali mbali za ujasiriamali zinazotolewa ili wajiendeleze kitaaluma na kujikwamua kiuchumi.
Nao washiriki wa mkutano huo wamesema watasimamia vyema majukumu waliopewa, na kusisitiza suala la uwazi na uwajibikaji kwa wadau wote wakati wa utekelezaji wa miradi ili kuijengea imani jamii juu ya miradi hiyo.