Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Ndugu Ali Abdulgulam Hussein amesema kutakiana kheri kwa kuombeana dua ni katika mambo ya kheri na kuimarisha umoja na mshikamano katika taasisi na jamii kwa ujumla.

Ameyasema hayo katika hafla ya kuwaombea dua mahujaji watarajiwa kutoka Wizara hiyo katika ukumbi wa Kituo cha Walimu Kiembesamaki Mjini Magharibi Unguja.

Mhe Gulam amewataka mahujaji hao watarajiwa kutumia fursa hiyo kuiombea dua nchi yetu hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa viongozi wakuu wa nchi.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Utawala Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Ndugu Khalid Masoud Waziri ameipongeza Wizara hiyo kwa mwenendo mzuri wa kila mwaka wa kuwaombea dua mahujaji watarajiwa na kuzitaka taasisi nyengine kuiga mfano huo kwani unaimarisha umoja na mapenzi kwa watendaji wa Taasisi.

Awali, akizungumza na hadhara hiyo Maalimu Siasa amewataka mahujaji watarajiwa kuwa wavumilivu na kuwa na subra katika kukabiliana na changamoto wakiwa katika kutekeleza matendo ya hija kwa kipindi chote watakachokuwa safarini.

Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano WEMA.