Mkuu wa divisheni ya Sekondari Ndugu Mfaume Jaffar Mfaume amewataka wanafunzi kuwa makini na kuyapokea mafunzo ya Stadi za maisha wanayopatiwa ili waweze kukabiliana vyema na mustakbali wa maisha yao baada ya kumaliza masomo.
Ameyasema hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Idara ya Elimu Sekondari wa Wizara hiyo Bi Asya Iddi Issa, wakati akifungua mafunzo ya Siku moja kuhusu Stadi za msisha kwa wanafunzi wa Sekondari kwa Wilaya saba za Unguja, katika ukumbi wa Kituo cha Walimu Kiembesamaki Mjini Magharibi Unguja.
Amewataka wanafunzi hao kuitumia vyema fursa hiyo ya mafunzo na kuwa mabalozi wazuri kwa wenzao ili lengo la serikali liweze kufikiwa.
Aidha Afisa Mfaume amewataka wanafunzi kufanya bidii zaidi katika masomo yao ikiwa ni jitihada za kumuunga mkono Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mainduzi Mhe Dkt Hussein Ali Mwinyi katika kunyanyua sekta ya Elimu nchini.
Hata hivyo amewanasasihi wanafunzi kutokujihusisha na masuala ya mapenzi na kuzingatia masomo yao pamoja na kuyatumia mafunzo wanayopatiwa kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili ili kutimiza ndoto zao.
Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano WEMA