Naibu Katibu Mkuu Utawala Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Ndugu Khalid Masoud Waziri Amesema habari ndio kitu pekee kinachopelekea jamii kujua Maendeleo yanayotekelezwa na taifa lao.
Amesema hayo wakati akifunga mafunzo ya kuwajengea uwezo Maafisa Habari na Uhusiano wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha utalii Maruhubi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Amesema iwapo maafisa wa habari watatekeleza wajibu wao ipasavyo itarahisisha upatikanaji wa taarifa kwa jamii kuhusu mambo yanayotekelezwa na serikali na kuondosha taarifa zisizo sahihi kutoka sehemu nyengine.
Aidha amewasisitiza maafisa hao kuhakikisha wanatumia lugha fasaha na taarifa zilizo sahihi ili jamii ifahamu mambo yanayotekelezwa na serikali yao katika sekta ya elimu. Pia amewasisitiza maafisa hao kujiendeleza kitaaluma ili kuhakikisha wanaendana na mabadiliko ya utoaji taarifa yanayoendelea duniani.
Nae Afisa wa kitengo cha habari na mawasiliano cha Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar ndugu Hafidh Kassim ameipongeza wizara kwa kuwajengea uwezo watendaji wake ili kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi.