Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Lela Muhamed Mussa ameshiriki katika hafla ya utiaji saini
Makubaliano (MoU) baina ya Karume Institute Of Technology (KIST) na Vocational Education and Training Authority (VETA) katika Ukumbi wa Mkutano wa KIST Mbweni - Mkoa wa Mjini Magharib.
Makubaliano hayo yana lengo la kuziwezesha Taasisi hizo mbili kushirikiana katika mambo mbalimbali ya Kielimu hasa katika kuandaa Walimu wa Ufundi.
Mapema Mhe. Lela amezitaka Taasisi hizo kuyasimamia kwa Ufanisi Makubaliano hayo ili yaweze kuleta tija kwa kuwaandaa Walimu wa Ufundi ili waweze kuwaandaa vyema Wanafunzi katika Masomo ya Amali.
Amesema, Walimu hao itakua chachu ya kufanikisha adhma ya Serikali katika utekelezaji wa Mageuzi ya Elimu nchini yenye lengo la kuwaandaa Wanafunzi kupata Ujuzi na kuweza kujiajiri na kupunguza changamoto za ajira nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Ufundi Stadi (VETA) Dkt. Prosper Lutangilo Mgaya amesema, katika kuyaendea Mageuzi hayo Makubwa ya Elimu Tanzania, ni lazma kuwepo kwa maandalizi mazuri ya Mitaala, Vifaa vya kufundishia na Walimu wenye Ubora ni nyenzo muhimu katika kuyafikia Mageuzi hayo na kuyasimamia kwa kuyafanyia kazi kwa muda mfupi.
Nae Mkuu wa Chuo Cha Ualimu Ufundi Cha Morogoro (MVTTC) Ndugu Samwel A. Kaali amesema, yuko tayari kutoa mashirikiano ya kutosha kupitia Uzoefu wa muda mrefu walionao na ameahidi kuyasimamia makubaliano hayo Kwa ufanisi mkubwa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa KIST Dkt. Mahmoud A. Alawi, amesema" Tuliona ipo haja ya kushirikiana na wenzetu kutoka VETA kupitia Chuo Cha Ualimu na Ufundi Stadi Morogoro Kwasababu wao wanauzoefu wa muda mrefu Ili tuweze kuzalisha Walimu mahiri na Weledi katika kuyafikia mahitaji ya upatikanaji wa Walimu wa Ufundi Stadi watakaoendana na Mabadiliko ya Mageuzi ya Elimu katika Mitaala Mipya ya Masomo ya Amali Kwa Zanzibar.