Waziri wa Afya Zanzibar Mh, Nassour Ahmed Mazrui amesema Mapinduzi ya Mwaka 1964, ndio siri ya Maendeleo ya Zanzibar kwani yameweza kupelekea kupiga hatua kubwa katika kuwaletea wananchi maendeleo. Ameyasema hayo katika Shamrashamra za kuadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar wakati alipokuwa akiweka jiwe la msingi Skuli ya Msingi Chumbuni Wilaya ya Mjini Unguja.
Mh, Nassour amesema ''kabla ya Mapinduzi hakukuwa na fursa sawa katika upatikanaji wa huduma za kijamii zikiwemo huduma za kielimu kwani Skuli zilikuwa chache na hivyo elimu ilikuwa ikitolewa kwa misingi ya kibaguzi na matabaka"
Aidha, ameeleza kuwa ujenzi wa miradi hiyo ya majengo ya Sekta ya Elimu ni ishara tosha ya kuthamini historia ya Mapinduzi yaliyoasisiwa na Mzee Abeid Aman Karume na kuitaka jamii iyungane na Serikali inayoongozwa na Dr Mwinyi ili kuenzi miradi ya kimaendeleo nchini
Pia ameushukuru Uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa jitihada zao wanazoendelea kuzichukua katika usimamizi na uboreshaji wa Sekta hiyo
Nae Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh, Ali Abdughulam Hussein amewataka walimu wayatumie majengo hayo ipasavyo na kuongeza jitihada ili kutimiza shabaha iliyokusudiwa. Aidha, ameiyomba jamii kuondoa hofu juu ya Serikali yao na watahakikisha changamoto za kielimu zinamalizika
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Ndugu Khamis Abdullah Said amesema Skuli hiyo mpya ya Msingi Chumbuni ni katika mikakati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuimarisha mazingira bora ya upatikanaji wa elimu ikiwa shabaha kubwa ni kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani na kufikia uwiano wa wanafunzi wasiozidi 45 kwa darasa moja na kuhakikisha madarasa ya kutosha yatakayopelekea skuli zote kuweza kuendeshwa kwa mkondo mmoja wa asubuhi badala ya mikondo miwili
Aidha, Ndugu Katibu wakati akitoa taarifa ya kitaalamu ya ujenzi wa Ghorofa 2 amesema Kampuni ya FUCHS inayojenga mradi huo inasimamiwa na Wakala wa Majengo ya Serikali (ZBA), itajenga Madarasa 29, Vyoo 25, Maabara za kisasa, Maktaba pamoja na Ofisi 4 utagharimu jumla ya fedha za Serikali TSh. 4,500,000,000/- kwa mujibu wa Mkataba
Nae Mkuu wa Wilaya ya Mjini Mh, Rashid Simai Msaraka amesema atahakikisha wilaya yake inazid kuwa na muonekano mpya hivyo jamii iyendelee kuunga mkono juhudi za Serikali kwa lengo la kufikia azma husika