Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya upatikanaji wa elimu bora kulingana na kasi ya ongezeko la watu Nchini.
Rais Dkt. Mwinyi amesema hayo katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi Skuli ya Utaani Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba ikiwa ni muendelezo wa shamrashamra za maadhimisho ya kilele cha miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Amesema kutokana na ongezeko la idadi ya watu Serikali imeimarisha mikakati yake na kuhakikisha kuwa hakuna Mzanzibar atakayekosa haki yake ya msingi ya kupata elimu popote alipo.
Aidha Rais Dkt. Mwinyi amesema katika kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira mazuri Serikali itahakikisha idadi ya wanafunzi darasani haizidi 45 sambamba na skuli zote kusomeshwa kwa mtindo wa Mkondo mmoja.
Amesema Serikali imeshapindukia agizo la Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa kujenga madarasa 2,273 badala ya 1500 kama ilivyoelekeza ilani hiyo kwa kipindi cha miaka mitano 2020 – 2025.