Afisa Mdhamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Mwalimu Mohamed Nassor Salim amekipongeza Kituo cha Elimu mbadala Wingwi kwa kutoa maarifa juu ya changamoto zinazoikabili jamii hali inayotoa hamasa kwasababu wanaungana na sera za nchi katika kuongeza fursa za kupata ajira.
Amesema hayo wakati wa ufungaji wa Mafunzo ya Siku mbili kwa Waalimu wa Kituo hicho yaliotolewa na Wakufunzi kutoka Tume ya Taifa UNESCO, katika Ukumbi wa Mikutano wa kituo hicho huko Wingwi Mkoa wa Kaskazini Pemba.
“Naamini kabisa kuwa mafunzo mliyoyapata yataboresha kwa kiwango kikubwa utendaji wenu wa kazi na kufanya kituo hiki kutekeleza kwa weledi jukumu lake muhimu sana la kuandaa vijana watakaoweza kujiajiri kwani jukumu mlilonalo ni kubwa sana kwa ustawi wa maendeleo ya nchi,” Amesema Mwalimu Mohammed.
Aidha amebainisha kuwa Mafunzo ya Elimu ya Ufundi Stadi yanagusa eneo muhimu sana la vijana, kwani vijana kupata elimu hiyo itawawezesha kuwa na aina mbali mbali za ujuzi katika utendaji kazi.
Ameongeza kuwa mafunzo ya ufundi yamesaidia kutoa maarifa kwa wananchi na kupelekea kujua fursa za ajira zilizopo katika maeneo yao.
Pia amesema mafunzo hayo yatasaidia wataalamu kuwa na maarifa yanayoendana na soko la ajira linalohitajika nchini.
Aidha amesema Wizara ya Elimu itaendelea kukiboresha kituo hicho kwa kurekebisha miundombinu mbalimbali ikiwemo manunuzi ya vifaa vya kufundishia na kujifunzia, na kuwajengea uwezo waalimu ili wawe na weledi katika kutekeleza majukumu yao.
Hata hivyo, Mdhamini huyo ametoa rai kwa Idara ya Elimu Mbadala na Watu Wazima Zanzibar kuendelea kuangalia mahitaji ya jamii ili waweze kuandaa mafunzo ya muda mfupi ili kuweza kuwapatia wananchi ujuzi utakao wasaidia kuzalisha ajira nyingi.
Kwa Upande wake Naibu katibu Tume ya Taifa UNESCO Bw. Aboud Khamis amesema, mafunzo hayo yamefanyika kutokana na utekelezaji wa programu shirikishi ambayo inafadhiliwa na Shirika la Utamaduni, Sayansi la Umoja wa Kimataifa(UNESCO ) ambayo lengo lake ni kuwajengea uwezo Walimu wa vituo vya Elimu Mbadala ili waweze kupata Marifa Mapya na Stadi zilizo bora wakati wa ufundishaji.
Kwa upande wao Washiriki wa Mafunzo hayo wameushukuru uongozi wa Idara ya Elimu Mbadala pamoja na Tume ya Taifa UNESCO kwa kuwapatia mafunzo hayo ya uboreshaji katika ufundishaji.