Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Abdulla, amewataka wazazi na walezi nchini kuendelea kuwaruhusu vijana wao kushiriki katika michezo, ili kuimarisha ufahamu katika mafunzo yao.

Amesema iwapo wanafunzi watashiriki kikamilifu katika michezo  wataweza kuongeza mbinu na kujiamini pamoja na kuimarisha akili zao wakati wa mafunzo.

Makamu wa Pili wa Rais ameeleza hayo wakati wa Kilele cha Tamasha la 59 la Elimu Bila Malipo 2023, hafla iliyofanyika katika Viwanja vya Skuli ya Sekondari Fidel Castro.

Aidha amewasihi wanafunzi hao kulinda na kuendeleza mila na silka za wazanzibari, wakati wote wanapokua katika michezo sambamba na kudumisha amani.

“Mwanafunzi anaposhiriki katika michezo kikamilifu, basi hata ufahamu wake katika masomo pia unaongezeka, ni wakati sasa wazazi kuwaruhusu watoto wao kushiriki katika michezo,”alisema.

Aidha amesema, Michezo hupelekea kuunda umoja, Ushirikiano, urafiki na udugu baina ya wachezaji, huku akiwasisitiza kuendelea kushiriki katika michezo kikamilifu.

Mapema Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe.Lela Muhamed Mussa, amesema, Tamasha la mwaka huu lilikuwa na ushindani mkubwa kutokana na michezo iliyoshindaniwa na skuli zilivyojipanga .

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Bw.Khamis Abdalla Said, amesema, msimu ujao watahakikisha wanaongeza mchezo mwengine mpya wa Criket, ili uweze kushindaniwa na kupatikana wachezaji wazuri.

Amesema, uwepo wa mchezo huo utaweza kuhamasisha wanafunzi nao kuanza kuupenda kama ilivyo michezo mengine, huku akiwataka vijana kujiweka tayari katika michezo.

Katika Tamasha hilo, Mkoa wa Kusini Pemba imefanikiwa kutwaa ubingwa wa mkoa wenye nidhamu, huku mkoa wa Mjini Magharibi ukatwaa mkoa bora wajumla katika
mashindano.


Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano (WEMA)
Tarehe:23/09/23