Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imesema, Itaendelea kuimarisha ushirikiano uliopo kati ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, ili kuwapatia elimu bora na yenye kukidhi mahitaji wanafunzi wa pande zote mbili.
Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Ali Abdul gulam Hussein, ameeleza hayo alipokuwa akizungumza na Walimu wa Jumuiya ya Walimu Wanawake wa Manispaa ya Morogoro waliofika zanzibar kwa ziara maalum huko katika Ukumbi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Mazizini Unguja.
Amesema, Malengo ya Waasisi wa Nchi ya Tanzania ni kujenga umoja ambao utaleta maendeleo katika nyanja mbali mbali za kiuchumi ambayo chimbuko lake ni elimu.
Aidha Mhe. Gulam amewakumbusha walimu hao kutembelea zaidi maeneo ya kihistoria kwa ajili ya kuitangaza vyema zanzibar ili wanafunzi wa huko nao wawe na hamu ya kutembelea zanzibar kutokana na utamaduni na vivutio vyake.
Nae Mwenyenyekiti wa Jumuiya ya Walimu Wanawake wa Manispaa ya Morogoro Bi. Brandina Joseph Mhai amesema, lengo la ziara hiyo ni kuweka mikakati ya kuhakikisha walimu wanamuangalia mwanafunzi kwanza katika ufaulu wake.
Walimu hao watatembelea katika maeneo mbali mbali ya kihistoria pamoja na baadhi ya skuli za elimu mjumuisho,skuli ya wanafunzi wanawake Benbela na kumalizia katika skuli ya Hasnuu Makame iliyoko Kibuteni Mkoa wa Kusini Unguja .
Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano (WEMA).
Tarehe:21/09/2023