Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib, amezindua rasmi tamasha la elimu bila ya malipo, na kuwataka wanamichezo kufanya michezo kwa amani, utulivu na mshikamano.


Amesema kuwekwa kwa Wanafunzi kutoka Mikoa yote mitano ya Zanzibar, kukaa sehemu moja kunapelekea kujuana, kuendeleza amani na mshikamano baina yao.


Mhe.Salama  ameeleza hayo katika viwanja vya michezo Chuo cha mafunzo ya amali Vitongoji Wilaya ya Chake Chake, wakati wa uzinduzi wa tamasha la 59 elimu bila ya malipo mwaka 2023 Kisiwani Pemba.


“Sisi viongozi wenu munaotuona hapa tupo kitu kimoja, sasa na nyinyi wanafunzi kuwepo kwenu hapa kutoka maeneo tafauti ni kuendeleza umoja, amani na mshikamano ndani yake,”amesema.


Aidha mkuu huyo amesema michezo ni afya, hujenga umoja na heshima, hivyo kushiriki michezo kwa wanafunzi isiwe sababu ya kwenda kinyume na maadili ya kizanzibari.


Aidha amewataka Wanafunzi kuhakikisha wanashiriki katika michezo ipasavyo, huku wakiweka mbele mavazi ya kizanzibari wakati wote wanapokua katika michezo.

Katika hatua nyengine mhe Salama, amewataka wasimamizi wa wanafunzi hao, kuwasimamia ipasavyo  katika suala zima la nidhamu, kwani haipendezi mtoto kukumbwa na matukio mabaya ambayo yataondosha heshima ya tamasha hilo.


“Kunatukio tunaendelea kulifatilia, asije akatokea mtu akayachezea maisha ya mtoto wa kike hapa, tutahakikisha watoto wote wanarudi kwao salama, likitokea tukio hilo basi mtu huyo tutakula nae sahani moja,”amesema.


Nae Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake Abdalla Rashid Ali, amesema ili Mwanafunzi aweze kufanya vizuri katika masomo yake, lazima pia ashiriki katika suala la michezo kikamilifu.


Kwa upande wake Afisa mdhamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba Mohamed Nassor Salim, amesema maandalizi yote ya tamasha hilo yameshakamilika hadi kufikia kilele chake Sepotemba 23 mwaka huu.


Mapema Mkurugenzi idara ya Michezo na Utamaduni kutoka Wizara ya Elimu Zanzibar Ahmed Abdalla Mussa, amesema tamasha hilo kwa mwaka huu limeshirikisha wanamichezo 2200 kutoka Unguja na Pemba, wakiwemo wanamichezo 30 wenye mahitaji maalumu.


Katika uzinduzi huo michezo mbali mbali imefanyika kiwanja cha Mapira Fidel Castro, Chuo cha Amani, Ngerengere Jeshini na Tenis Chake Chake, kwa mpira wa miguu, Hand boll, basket Boll, Netboll na Volboll.