Mratibu Idara ya Utumishi na Uendeshaji Mwalimu Harith Bakar Waziri amesema kisomo cha Watu Wazima ni njia muhimu ya Kuwakomboa na Kutokujua kusoma, kuandika na kuhesabu.

Ameyasema hayo katika kikao cha Kutathmini Maendeleo ya Kisomo cha Watu wazima kilichowashirikisha Wanakisomo kutoka Wilaya nne za Pemba ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za Maadhimisho ya Juma la Kisomo cha Wtu wazima Huko katika Ukumbi wa Wizaraya Elimu na Mafunzo ya Amali Chake Chake Pemba.

Mwalimu Harithi amesema wakati dunia ikiadhimisha Wiki ya Kisomo kuna haja kubwa ya kutathmini maendeleo yaliyofikiwa katika kuwakomboa watu kuondokana na tatizo la kutokujua kusoma, kuandika na kuhesabu.

Akifafanua zaidi Mratibu huyo amesema kufanyika kwa Tathmini hio kutasaidia kujua ufahamu wa Wanakisomo hao  na namna ya kuweza kuwasaidia.

Aidha amewataka waratibu wa Kisomo cha Watu wazima pamoja na Walimu wanaowafundisha kisomo hicho kutumia lugha nzuri pamoja na kuwapa mashirikiano Wanakisomo hao.

Nae Mratibu Idara ya Elimu Mbadala na Watu Wazima Nd. Salim Kuza Sheikhan amewataka wanakisomo cha Watu wazima kutorudishwa nyuma na maneno ya kukatisha tamaa yanayosemwa na  ya baadhi ya Wanajamii.

Amesema kuna baadhi ya Wanajamii wanaona kisomo cha Watu Wazima nikupoteza muda na kudhalilika jambo ambalo Mratibu huyo amesema sio sahihi badala yake ni ukombozi kwa waliokosa huduma hiyo katika umri wao wa utotoni.

Amesema kufanyika kwa tathmini hio ni njia moja wapo ya kupiga hatua moja mbele kwa Wanakisomo nakuweza kufahamu maeneo ambayo wanapaswa kuongeza juhudi zaidi katika kujisomea.

Akisisitiza juu ya Umuhimu wa  kisomo hicho amesema nivyema wanakisomo hao kufanya bidii zaidi kwani kufanya hivyo nikuunga mkono jitihada za Raise wa Zanzibar  Dkt. Husein Ali Mwinyi katika sekta ya Elimu.

Kwa Upande wake Afisa Kisomo cha Watu Wazima Nd. Haji Juma Haji amesema Idara inaendelea kufanya upembuzi yakinifu kubaini maeneo ambayo yanamahitaji zaidi ya kufunguliwa kwa madarasa mapya ya Kisomo cha Watu wazima.

Shamrashamra za Maadhimisho ya Juma la Kisomo cha Watu Wazima kwa Upande wa Pemba zilizinduliwa rasmi kwa shughuli za usafi katika Hospitali ya Wilaya Vitongoji ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni “Kukuza Uwezo wa Kusoma na Kuandika kwa Mabadiliko ya  Ulimwengu ili Kujenga Misingi ya Jamii Endelevu na Yenye Amani”