Wanafunzi wa Skuli za Sekondari wametakiwa kuwa wabunifu ili waweze kukabiliana na changamoto mbali mbali katika maisha na kuweza kusoma kwa bidii.

 

Wito huo umetolewa na Mratibu ldara ya Elimu Mbadala na Watu Wazima Mw. Salum Kuza Sheikhani wakati akifungua mafunzo ya siku tano ya kuwajengea Wanafunzi uwezo wa matumizi ya Teknilojia ya karne ya 21 (2021 century skulls) Yaliyowashirikisha Walimu na Wanafunzi wa Skuli za Sekondari huko katika Ukumbi wa Skuli ya Hemedi Suleiman Pujini Wilaya ya Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba.

 

 

Mw. Salum amewataka Wanafunzi hao kutumia fursa ya Mafunzo hayo katika kufanya ubunifu kupitia nyanja mbalimbali ikiwemo elimu, afya kilimo pamoja na mawasiliano.

 

 

Aidha amesema Mafunzo hayo yanalenga kuwapatia muelekeo chanya hivyo amewataka Wanafunzi hao kuyashikilia vyema mafunzo hayo amabayo yatawajengea uwezo kivitendo na kiubunifu zaidi.

 

Akitoa shukurani kwa Taasisi ya Milele Zanzibar Foundation Mw. Salum amesema Taasisi hiyo inatoa mchango mkubwa katika sekta ya elimu hivyo ameiomba kuendelea kufanya hivyo ili kuendeleza mbele gurudumu la elimu Nchini.

 

Kwa upande wake Meneja wa Taasisi ya Milele Zanzibar Foundation Ndg. Abdallah Saidi Abdallah amesema mafunzo hayo yatawaandaa Wanafunzi katika kukabiliana na mazingira ya skuli na nje ya skuli.

 

Akifafanua zaidi Ndg. Abdallah amesema dunia inakwenda sambamba na mabadiliko ya kiteknolojia hivyo Milele Zanzibar Foundation itaendelea kutoa programu za kitaaluma kwa Wanafunzi ili waweze kuyakabili mazingira yao.

 

Nae Mkufunzi wa mafunzo hayo bi Raya Idrisa Ahmad amewataka wanafunzi waache kujifunxa kimaxowea na badala yake wajenge tabia ya kuwa wadadisi kwa kuwa mafunxo haya yatakwenda kutatua changamoto mbali mbali wanazokabiliana nazo katika jamii.