Shirika  la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) linatarajia kulifanyia matengenezo makubwa jengo la Majestic cinema la Mji mkongwe na kuwa kituo kikuu cha utamaduni.

 

Akizungumza  katika warsha ya siku mbili yenye lengo la kujadili mikakati ya kulitengeneza jengo hilo kati ya wataalamu wa UNESCO na watendaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe. Lela Muhamed Mussa amesema, hatua hiyo itaongeza fursa kwa Zanzibar na kuimarisha sekta ya utalii kutokana na kuutunza Mji mkongwe na kuongeza hadhi ya vivutio vyake.

 

Awali ya hapo mwakilishi wa UNESCO nchini Tanzania Michel Toto amesema UNESCO itaendelea kuiunga mkono Serikali ya Zanzibar katika kuyafikia malengo yake ya kuuhifadhi mji huo ili uweze kuleta manufaa zaidi kwa kizazi cha sasa na kijacho.

 

Naye balozi wa Japan nchini Tanzania Yasushi Misawa na balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania bwana Yahya bin Ahmed Okeish  wamesema kupitia UNESCO watasaidia kufanikisha utekelezaji wa mradi wa kulikarabati jengo la Majestic Cinema lenye historia ya muda mrefu visiwani Zanzibar.

 

Kwaupande wake Mkurugenzi wa taasisi ya Hifadhi Zanzibar Tonino Sarav amesema licha ya taasisi hiyo kutafuta ufadhili wa kuikarabati Majestic Cinema itahakikisha inasimamia mradi wa ujenzi wa jengo hilo pamoja na uendeshaji wake.

                

Jengo  la Majestic Cinema awali  lilijengwa mnamo mwaka 1921 ambapo watu kutoka maeneo mbalimbali walikutana kuangalia filamu na kubadilishana uzoefu na baadae kujengwa tena baada ya kuungua moto mnamo mwaka 1951.

 

Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar (WEMA).