Ufanyaji wa tafiti za kielimu utapelekea kuibua changamoto pamoja na kubuni mikakati na mipango madhubuti ya kielimu itakayosaidia kuinua sekta hiyo kwa maslahi mapana ya maendeleo ya kielimu nchini.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Bwana Khamis Abdulla Said wakati akifungua kongamano la siku moja la uwasilishaji wa matokeo ya utafiti uliofanya na Shirika la UNICEF ujulikanao kama  Data Must Speak (DMS)katika Ukumbi wa Golden Tulip Uwanja wa ndege Wilaya ya Magharibi B Unguja.

Bwana Said amesema kuwa utafiti ni muhimili muhimu kwa ustawi wa Wizara na ndiyo dira inayoakisi mustakabali wa mafanikio na maendeleo ya kielimu katika taifa kwa kuwa mipango yote ya kielimu hupangwa baada ya kufanyika kwa tafiti za kina ambazo hutumika na watunga sera ili kuliongoza taifa katika mwelekeo ulio sahihi.

Aidha Katibu Mkuu ameishukuru na kuipongeza UNICEF pamoja na wale wote walioshiriki kufanikisha mradi huo kwa kujitolea kwao kwa hali na mali na kuongeza kuwa matokeo ya utafiti huo yatasaidia kupanga mipango sahihi ya kielimu ili kuwasaidia watoto kuondokana na changamoto zinazowakabili katika nyanja za kielimu.

Awali akiwasilisha matokeo ya utafiti huo mwakilishi wa UNICEF bibi Erica Aiazzi lieleza kuwa utafiti huo umehusisha skuli kumi na nane zikiwemo kumi kutoka Unguja na nane kutoka Pemba ambapo utafiti huo ulifanywa kwa kuangalia mkengeuko chanya “Positive Deviance” kwa skuli ambazo zina mazingira yanayofanana.

Tafiti za DMS za UNICEF kwa sasa zimeshatekelezwa katika nchi kumi na nne na Tanzania ikiwa ni miongoni mwa nchi hizo ambapo kwa upande wa Tanzania bara tayari matokeo ya utafiti huo yameshachapishwa.

Imetolewa na kitengo cha habari Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Zanzibar.