Utekelezaji wa Mikutano ya Tathmini ya Elimu ya Zanzibar ni kilelezo tosha cha Serikali inayozingatia misingi ya utawala bora katika kuwaongoza na kuwaletea maendeleo wananchi wake katika nyanja mbali mbali ikiwemo Sekta ya Elimu.

Amesema hayo Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Lela Muhamed Mussa , Wakati alipofungua Mkutano wa Saba wa Tathmini ya Sekta ya Elimu, katika Ukumbi wa Madinat Al Bahar , Mbweni - Zanzibar.

 

  Amesema, Elimu ndio msingi bora wa maendeleo hivyo ni vyema kuendeleza mashirikiano ya karibu ili kuhakikisha Sekta ya Elimu inaimarika zaidi.

 

Aidha amewataka Washiriki kuisimamia vyema ajenda ya mageuzi ya elimu pamoja na kuhakikisha urasimu hauchukui nafasi katika utekelezaji wa mageuzi ya elimu.

 

Amesema, lengo la Mageuzi ya Elimu ni kuhakikisha Elimu inayotolewa Zanzibar inaendana na mahitaji ya karne ya 21 kwa kuzalisha vijana wenye uwezo wa kufikiri kwa kina.

 

Amesema, Mkutano huo ni jukwaa muhimu la kuweza kuyatathmini mafanikio na changamoto pamoja na kupanga mikakati imara kwa kipindi kijacho .

 

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Ndugu. Khamis Abdulla Said amesema, Mkutano huo unaofanyika kila mwaka unalengo la kujitathmini na kujadili mafanikio na changamoto mbalimbali ya Elimu na kupanga mikakati imara katika kuyaendea Mageuzi makubwa ya Sekta ya elimu kwa mafanikio makubwa.

 

 

Nae Mwenyekiti wa Kamati ya Ustawi wa Jamii wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Sabiha Philphil Thun, ameipongeza Wizara ya Elimu kwa kufanya Tathmini ya Elimu kwa kila Mwaka hali ambayo itatoa mwanya wa kurekebisha mapungufu yaliyopo na kuboresha zaidi Sekta hii ya Elimu.

 

Hata hivyo Mhe. Sabiha ameahidi kuendelea kutoa mashirikiano katika kuwajengea uwezo walimu na kusaidia vifaa mbalimbali katika Sekta ya Elimu.

 

 

Akitoa salamu za shukran Mwakilishi kutoka Asasi za Kiraia Ndugu Salim Ali Salim. ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya usimamizi wa Wizara ya Elimu kwa mashirikiano wanayotoa kwa Sekta Binafsi, jambo ambalo linatoa fursa Kwa Wadau mbalimbali kuweza kuekeza katika Sekta ya Elimu.  

 

 

Nae Mwakilishi kutoka kwa Wadau wa Maendeleo Ndugu. Micko Toto ameeleza kuwa, Bado kuna changamoto mbalimbali katika Sekta ya Elimu ikiwemo, uwezo wa kutumia teknolojia katika kujifunza sambamba na utumiaji wa mbinu shirikishi katika kujifunza. 

 

Hivyo ameahidi kusaidiana na Serikali katika kuhakikisha Mageuzi makubwa ya Elimu yanafanikishwa kwa ufanisi mkubwa.