Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema, Serikali itaendelea kushirikiana na Wadau mbalimbali ikiwemo Benki ya Dunia, kwani wamekuwa wakiunga mkono katika kuwaletea maendeleo wananchi wake.

Akizungumza katika uzinduzi wa mradi wa kuimarisha ubora wa elimu ya Lazima  Zanzibar (ZIQUE).Hafla ambayo imefanyika katika kiwanja cha skuli ya Salim Turky Mpendae Mjini Unguja, 

Amesema, WB kwa muda mrefu imekuwa ikisaidia kwenye maeneo mbalimbali hasa katika eneo la huduma za jamii ikiwemo Miradi ya 'Zanzibar Basic Education Improvement Poroject' (ZABEIP) iliogharimu dola za kimarekani milioni 42, mradi wa 'Zanzibar Improving Student Prospects' (ZISP) dola za kimarekani milioni 35 pamoja na mradi wa 'Zanzibar Improving Qualit of Basic Education'  (ZIQUE) uliotengewa jumla ya dola za kimarekeani milioni 50.

Amesema, Miradi hiyo pamoja na miradi mengine imeleta mafanikio makubwa ikiwemo kuimarisha mazingira ya kujifunzia ya kufundishia yaliyopelekea kuimarika kwa ufaulu wa wanafunzi katika mitihani yao ya taifa hasa katika masomo ya sayansi.

Aidha amesema, miradi hiyo imesaidia kufikisha huduma ya elimu katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo katika visiwa vidogo vidogo Unguja na Pemba ikiwemo Tumbatu Kojani, Fundo, na Kisiwapanza.

"Mradi huu umekuja wakati muafaka ambao Serikali inajipanga kutekeleza mageuzi makubwa ya sekta ya elimu kama yalivyopendekezwa na ripoti ya kikosi kazi" amesema.

Aidha amesema kuwa, utekelezaji wa mageuzi hayo utachangia pia ubora wa elimu inayoendana na mahitaji ya sasa ya ulimwengu itasaidia kuwaandaa vijana katika fani mbalimbali na hivyo kuchangia kutimiza dira ya maendeleo ya kuwa na uchumi wa kati kiwango cha juu ifikapo mwaka 2050 kama ilivyoelekezwa katika dira ya maendeleo ya Zanzibar ya mwaka 2050.

Hata hivyo, amesema kuwa, Serikali imeweka mkazo mkubwa katika kuimarisha elimu kwa kupambana na changamoto zinazoikabili sekta ya elimu kwa kutatua changamoto zilizoikabili sekta hiyo kwa kuwajengea uwezo na ujuzi ulio sahihi vijana kwa kuwapatia taaluma mbalimbali.

Hivyo, ameuomba Uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, kusimamia vvyema utelelezaji wa mradi huo na mengine katika utekelezaji wa miradi kwa kutekeleza kwa muda uliopangwa na kuwataka wananchi kuendelea kuitunza miundombinu inayojengwa na serikali ambapo kufanya hivyo ni kuthamini jitihada za serikali.

Nae, Waziri Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Dk. Sada Mkuya, amesema, wataendelea kushirikiana na sekta zote kutafuta rasilimali fedha za ndani na mashirika ya maendeleo katika kutekeleza shughuli za kiuchumi na kijamii.

Amesema, kupitia mradi huo ambao wameshirikiana bega kwa bega na Wizara ya Elimi na kuhakikisha mradi huo na kusema kuwa kupitia miradi hiyo wameweka miadi ya utekelezaji kwa muda wa miaka mitatu kwa mujibu wa dhamira na miongozi ya utekelezaji upo.

"Mradi huu tutautekeleza kwa muda wa miaka mitatu tutakamilisha mambo yote na fedha nyengine inakuja ipo njiani" amesema.

Mapema akimkaribisha mgeni Rasmi Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe. Lela Muhamed Mussa, amesema, Wizara itaendelea kuwaunga mkono washirika mbalimbali kwani wamekuwa wakiwawezesha kwa kila mwaka kupitia sekta ya elimu.

Aidha ameahidi kuendelea kufanya kazi kwa mashirikiano makubwa na kufanya kazi nao usiku na mchana ili lengo liweze kufikiwa na kusema kwa mwaka huu kwa mara ya kwanza wanafunzi wote wamefaulu kwenda vyuo vikuu.

Amesema, kwa niaba ya wizara ameishukuru Serikali, kwani imekuwa ikitafuta rasilimali fedha na ujuzi hivyo waliahidi kusimamia na maagizo na maoni ya Rais wa Zamzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi anayoyataka kuyaona kupitia sekta ya elimu yanakwenda kwa vitendo.

Nae, Mwakilishi wa Benki ya Dunia nchini Tanzania, Nathan Balete, amesema, WB imekuwa ikiunga mkono jitihada za Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kwani wamekuwa na jitihada za kuona elimu inakuwa Tanzania.

Sambamba na hayo, amesema kuwa, mradi huo utanufaisha wanafunzi na ukuaji wa Uchumi wa nchi kupitia mradi huo.

"Tutaendelea kuiunga mkono serikali zote mbili hasa katika sekta ya elimu kwani elimu ndio msingi wa kila kitu katika kuleta maendeleo" amesema, 

Nae Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Zanzibar Bw.Khamis Abdallah Said, amwsema, Mradi huo unatekelezwa kwa mashirikiano na Benki ya Dunia na utatekelezea kwa kipindi cha miaka mitatu.

Aidha amesema, mradi huo utagharimu milioni 50 za kimarekani na lengo kuu ni kuona ufaulu unaengezeka na mfumo wa elimu unaweza kuzalisha wasomi waliokuwa wazuri nchini.

Aidha amesema, Mradi huo utatekelezwa kwa vipengele mbalimbali ikiwemo kuwajengea walimu uwezo ili kuimarisha ufanisi wa kazi yao katika kusomesha kwa kufuata mitaala ya unahiri.

Nae, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Idrisa Kitwana Mustafa, amesema, Rais Dk. Mwinyi amekuwa akiwekeza katika elimu hivyo, amesema, wataendelea kushirikiana nae ili kuona watoto wa Zanzibar wanakuwa na elimu iliyokuwa bora zaidi.

"Wananchi wanakushukuruni sana viongozi wao na huu mradi utakwenda kuondoa changamoto kwani magorofa sita yatajengwa katika mkoa wetu huu kupitia mradi huu na pia  utaenda kuondoa ukakasisi wa kuona vijana wetu wanakwenda kusoma katika mazingira mazuri zaidi" amesema.


Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano (WEMA).
Tarehe:26/09/2023