Serikali kupitia wizara ya elimu inafanya kila jitihada ili kuhakikisha inaondosha kabisa alama ya zero kwenye  matokeo ya kidato cha nne.

Amesema hayo Mkurugenzi Idara ya Elimu Sekondari Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar bi Asya Iddi Issa wakati wa mkutano na Walimu Wakuu wa Skuli zenye Wanafunzi wengi wa kidato cha nne katika ukumbi wa Mikutano wa Mazizini Unguja. 


Akizitaja skuli ambazo  zinaongoza kuwa na wanafunzi wengi amesema ni skuli ya  Mwanakwerekwe C 410, Mtopepo  416, Kinuni 400 , na Nyerere 483.


Amesema idara yake ipo sambamba na Walimu hao ili kuendelea na mikakati ya kuhakikisha  Skuli hizo nazo zinaondoa kabisa alama ya zero.


Bi Asya amesema kutokana na changamoto ya wingi wa wanafunzi kwenye baadhi ya Skuli za Mkoa wa Mjini Magharibi  idara kwa kushirikiana na  Walimu hao   wataendelea na bidii  kuhakikisha  wanafunzi wote wanapata ufaulu mzuri na kuondosha kabisa alama ya zero.


Aidha bi Asya amesema  wazazi nao wananafasi ya kushikiana na walimu ili kuhakikisha jitihada hizo zinapelea wanafunzi  matokeo mazuri.


Pia Mkurugenzi Asya amewataka walimu hao kuhakikisha wanadhibiti utoro kwa  kuchukua hatua na  kupeleka taarifa kwa Katibu Mkuu ili zichukuliwe hatua kama ilivyoelezwa na   baraza la Mtihani Tanzania (NECTA) na kuhakikisha taarifa hizo ziwe sahihi na ziwe na vielelezo vilivyojitosheleza.


Nao walimu walioshiriki kikao hicho wamesema utoro ni changamoto  kubwa kwa wanafunzi hao na kupelekea wao kupata matokeo mabaya.


Wamesema utoro huo huzidi  kipindi ambacho  wanafunzi kusajiliwa na kuhakikisha watafanya mtihani wa taifa

 

Kikao hicho cha tatu kimefanyika leo tarehe 13/09/2023  ni muendelezo  wa kuweka  mikakati ya kuondosha alama ya zero hasa katika skuli zenye idadi kubwa ya wanafunzi.