Title Image

WAZIRI WA ELIMU AWAOMBA WAZEE/WALEZI NA MADEREVA KUWASAIDIA WATAHINIWA.

news phpto

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe. Riziki Pembe Juma akizungumza na vyombo vya habari juu ya taarifa kwa Umma kuhusu ufanyikaji wa mitihani ya Taifa ya SMZ kwa mwaka mwaka 2017

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe Riziki Pembe Juma ametoa taarifa ya ufanyikaji wa Mitihani ya Taifa kwa upande wa Zanzibar itakayofanyika tarehe 20, Novemba 2017 hadi tarehe 5, Disemba 2017.

Waziri Riziki ametoa taarifa hiyo leo Ofisini kwake, Mazizini na kusema jumla ya watahiniwa 124,190 wakiwemo wanawake 65,272 na wanaume 58,918 wamesajiliwa kufanya mitihani hiyo sawa na ongezeko la asilimia 25.49 ukilinganisha na watahiniwa 98,963 waliosajiliwa mwaka 2016.

Alisema ongezeko hilo limekuja kutokana na makundi wawili ya watahiniwa wa kidato cha pili waliomaliza msingi mwaka 2015 wale ambao walimaliza Darasa la saba na Darasa la Sita kwa mwaka 2016.

Pia alisema kwa mwaka 2017, jumla ya watahiniwa 40,201 ambao wanawake ni 19,948 na wanaume ni 20,253 wamesajiliwa kufanya mtihani wa Darasa la nne sawa na ongezeko la asilimia 3.74 ukilinganisha na mwaka 2016.

Kwa mtihani wa Darasa la Sita watahiniwa 34,456 wamesajiliwa kufanya mtihani huo wakiwemo wanawake 18,072 na wanaume 16,384 sawa na ongezeko la asilimia 3.50 ikilinganisha na mwaka Jana 2016.

Aidha watahiniwa 49,533 wamesajiliwa kufanya mtihani wa kuingia kidato cha tatu kati yao wanawake 27,252 na wanaume 22,281 sawa na ongezeko la asilimia 45.46 ukilinganisha na mwaka 2016.

Aidha Waziri Riziki aliwaomba wazazi/walezi na wananchi wote kwa jumla kuwa karibu zaidi na watoto wao wanaofanya Mitihani ili kuhakikisha wanafika mapema katika vituo vyao vya kufanyia mitihani na kuwataka madereva na Utingo wa Gari za abiria kuzidisha busara na hekima kwa wanafunzi katika vyombo vya usafiri wakati wa kwenda na kurudi kutekeleza haki yao ya msingi ya Elimu.

Pia alisisitiza amani na utulivu katika mitihani hiyo kwa watahiniwa na kwamba mtu yoyote asiyehusika asijaribu kusogelea Kituo cha mtihani kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na Sheria na Kanuni za Mitihani.

Hivyo yoyote atakayepatikana na hatia, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake aidha watahiniwa wametakiwa wote kujiepusha na vitendo vyovyote vya udanganyifu kwani yoyote atakaye bainika kufanya hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake pamoja na kufutiwa matokeo yake.

Hata hivyo Waziri ametangaza rasmi kuzifunga kambi zote za kujiendeleza zilizowekwa ndani ya skuli za Serikali na Binafsi na zilizowekwa nje ya skuli.