Title Image

Dk. Shein Aupongeza Uongozi wa Wizara ya Elimu

news phpto

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akizungumza na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali katika utekelezaji wa mpango kazi wa Wizara kwa kipindi cha mwaka 2016/17, mpango kazi wa mwaka 2017/18 na utekelezaji wa robo ya kwanza Julai - Sept, 2017

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, ameupongeza uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa kutekeleza vyema majukumu yake na kusisitiza kuwa lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni kuwa na elimu bora.

Hayo aliyasema leo, Ikulu mjini Zanzibar alipokutana na uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali wakati ilipowasilisha utekelezaji wa Mpango Kazi wa Mwaka 2016/2017, Mpango Kazi wa Utekelezaji kwa mwaka 2017/2018 na Utekelezaji wake kwa kipindi cha robo ya kwanza ya Julai hadi Septemba kwa mwaka 2017.

Aidha, Dk. Shein aliueleza uongozi huo haja ya kufanya kazi kwa pamoja, kusaidiana na kushirikiana katika kutekeleza majukumu yao ili Wizara hiyo ienndelee kupata mafanikio makubwa zaidi na kuwasisitiza kuwa wasichelee kuchukua hatua pale inapobidi kufanya hivyo bila ya kumuonea mtu yeyote.

Mapema akizungumzia suala la utafiti, Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya kuwepo kwa tafiti katika Wizara kwani hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuibua mambo mbali mbali na hatimae kupata majibu na kueleza kuwa Wizara yoyote ya Serikali haiwezi kwenda bila ya kufanya tafiti.

Dk. Shein pia, alisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa vuguvugu la mashindano ya riadha kwa wanafunzi katika kipindi cha sherehe za Elimu Bila Malipo kwa lengo la kuibua vipaji.

Alieleza kuwa ni vyema kwa kila mwanafunzi akapata muda wa kucheza na kuweza kushindana na wanafunzi wenziwe katika skuli nyengine ili wawe wakakamavu na kusisitiza haja ya kila skuli kuwa na mwalimu maalum wa michezo kama ilivyokuwa hapo siku za nyuma.